VPL: Mbao wachapwa na Singida, Simba mwendo mdundo

VPL: Mbao wachapwa na Singida, Simba mwendo mdundo

07 Feb, 18:24

Ligi kuu soka Tanzania Bara imeendelea Jumatano ya Februari 7 katika michezo mitano kupigwa katika viwanja mbalimbali nchini.

Jijini Mwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeambulia kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Singida United, katika mchezo ambao mabao mawili kati ya matatu yakifungwa kwa penati.

Kila timu iliuanza mchezo huo kwa tahadhali kubwa ikijaribu kutofanya makosa ya mapema ambayo yangeweza kuwagharimu.

Hata hivyo ndani dakika 10 za mwanzo tayari Mbao walikuwa wamefika langoni mwa Singida United mara mbili lakini mara zote Habibu Haji Kiyombo alikosa umakini kuweza kutumbukiza mpira wavuni.

Dakika ya 22 Mbao walipanda kwa kasi langoni mwa Singida United wakati ambapo mabeki walikuwa bado hawajajipanga vizuri na Ismail Ally alipiga shuti na likaokolewa na kipa Ally Mustapha.

Mbao walilitawala dimba la uwanja wa CCM Kirumba wakicheza Pasi fupifupi ambazo kwa umahiri mkubwa waliwachanganya wachezaji wa Singida United.

Katika dakika ya 45 Singida United walipata penati baada ya Mpira wa kona uliopigwa na Deus Kaseke kuonekana kumgonga mkononi Nahodha wa Mbao Yusuph Ndikumana.

Penati hiyo ilienda kuchongwa na Shafik Batambuze na yeye bila kinyongo akautia mpira wavuni na kuwaandikia Singida United bao la kuongoza.

Kipindi cha pili Mbao walianza kwa kuwatoa Wacheza wawili James Msuva na Abubakar Ngalema na kuwaingiza Abdulkarim Segeja na Herbert Lukindo ili kuongeza mashambulizi.

Mabadiliko hayo yalisaidia Mbao ambao walianza kucheza kwa kasi na kulishambulia lango la Singida United Kama nyuki na hatimaye dakika ya 50 walipata penati baada ya Abdulkarim Segeja kufanyiwa madhambi ndani Michelle Rusheshangoga ndani ya 18.

Penati hiyo ilienda kuchongwa na Habibu Kiyombo na bila ajizi akamchambua kipa Ally Mustapha na kuiandikia Mbao bao la kusawazisha.

Hata hivyo bao hilo halikudumu sana, katika dakika ya 58 mlinzi wa Mbao David Mwasa alifanya Makosa akijaribu kuuokoa mpira lakini akaukosa na kumkuta Deusi Kaseke anbaye hakujiuliza sana na kuandika bao la pili kwa Singida United.

Licha ya kosakosa za hapa na pale lakini hadi dakika 90 zinamalizika Mbao ambao ndio walikuwa wenyeji walitoka vichwa chini kwa kufungwa kwa mabao 2-1.

Vikosi vilivyocheza.

Mbao: Matacha Mnata 33, Vincent Philipo 9, Amos Abel 25, David Mwasa 4, Yusuph Ndikumana 14, Ibrahim Njohole 22, Abubakar Ngalema 19/Abdulkarim Segeja, Hussein Kasanga 8, Habibu Haji Kiyombo 17, Ismail Ally 7/ Emmanuel Mvuyekule, James Msuva 13/ Herbert Lukindo.

Akiba: Yvan Rugumandiye 1, Ally Kombo 6, Emmanuel Mvuyekule 10, Said Khamis 3, Abdulkarim Segeja 2, Seleman Bwelle 29 na Herbert Lukindo 22.

Singida United: Ally Mustapha 30, Michael Rusheshangonga 22, Shafik Batambuze 6, Malik Antiri 3, Salum Kipaga 5, Mudathir Yahya 27, Deus Kaseke 7/Kiggy Makasi, Yusuf Kagoma 21, Lubinda Mundia 11/Tafadzwa Kutinyu, Kenny Ally 8 na Salumu Chuku 12.

Akiba: Said Lubawa 1, Miraji Adam 24, Kiggy Makasi 4, Mohamed Abdallah 26, Assad Juma 13, Ally Ng'anzi na Tafadzwa Kutinyu 20.

Matokeo mengine. 

FT: Simba 1-0 Azam FC - Taifa, Dar es Salaam.

FT: Stand United 0-3 Lipuli FC - CCM Kambarage, Shinyanga.

FT: Mwadui 3-1 Mtibwa Sugar - Mwadui Complex, Shinyanga.

FT: Majimaji 0-0 Tanzania Prisons - Majimaji, Ruvuma.

FT: Ndanda 2-2 Mbeya City - Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Related news
related/article
International News
UEFA CL: Real Madrid v Liverpool the key battles
22 hours ago
International News
Koscielny reveals his remedy to World Cup heartache
24 May, 16:40
Betting Previews
UEFA CL Final preview: Real Madrid vs Liverpool-Prediction, team news & line-ups
23 May, 12:00
International News
Xavi 'thrilled' to sign two-year Al Sadd extension
24 May, 21:06
International News
Liverpool working to help fans after flight cancellations
24 May, 21:33