VPL: Simba, Azam watupiana tambo, rekodi zinasemaje?

VPL: Simba, Azam watupiana tambo, rekodi zinasemaje?

07 Feb, 09:09

Ligi kuu soka Tanzania Bara inaendelea Jumatano hii kwa michezo mitano lakini mechi ambayo inateka fikra na mawazo ya wengi ni ile kati ya mnyama Simba SC na Azam FC.

Tayari kila timu imetoa tambo zake kuelekea mchezo huo ambao utafanyika kwenye uwanja mkubwa na wa kisasa nchini, uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Tukianza na wenyeji Simba SC, msemaji wao Haji Manara amesema wanatambua ugumu wa mchezo huo na ndio maana wamefanya maandalizi makubwa, ukizingatia kwamba wao wanahitaji pointi tatu zaidi.

"Ni Mechi Ngumu, kila timu imejiandaa, Azam wanawachezaji wazuri sana na ni wachezaji wakubwa, very professional club lakini sisi tunahitaji pointi tatu, kuweza kuendelea kuongoza ligi kuu" ameeleza.

Kwa upande wake Jaffary Idd Maganga ambaye ni afisa habari wa Azam amesema wanashukuru baadhi ya wachezaji wao wamerejea tayari kucheza na Simba.

"Mwalimu ameandaa kikosi kizuri kabisa ambacho kitawapa furaha mashabiki, wachezaji wote ni wazima ukiondoa wawili tu Waziri Junior na Joseph Kimwaga, lakini Stephen Kingu na wengine wamerejea," Maganga amesema.

Rekodi muhimu 

Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 19 kwenye mechi za ligi tokea Azam FC ipande mwaka 2008, matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wakishinda mara tano, Simba wakiibuka kidedea mara nane na ikishuhudiwa mechi sita wakienda sare.

Aidha kwenye mechi za mashindano yote zimekutana mara 28, Azam FC ikishinda mara 10, Simba mara 12 huku mechi sita zikienda sare, hiyo inajumuisha mechi za ligi, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), Kombe la Kagame, Kombe la Ujirani Mwema, Kombe la Banc ABC Super 8 na Ngao ya Jamii.

Kwa msimu huu, hiyo itakuwa ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana, katika mechi mbili zilizopita Azam FC ikishinda mmoja kwenye Mapinduzi Cup bao 1-0, lililofungwa na winga Idd Kipagwile huku ule wa ligi raundi ya kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex ukiisha kwa suluhu.

Wachezaji muhimu 

Nahodha wa zamani wa mafanikio wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, aliyehamia Simba msimu huu ndiye kinara wa kufunga mabao mengi kwenye mchezo baina ya timu hizo, akitupia wavuni mara 19 yote akifunga wakati yupo Azam FC, na anatarajiwa kucheza dhidi ya timu yake ya zamani hiyo kwa mara ya tatu msimu huu.

Hadi sasa ikiwa inaelekea raundi ya 17, wachezaji wanne wa Azam FC wamefunga zaidi ya bao moja kwenye ligi, Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph, wawili hao wakiwa kileleni ndani ya timu hiyo kila mmoja akifunga matatu huku Shaaban Idd na Paul Peter, nao kila mmoja akifunga mawili.

Simba hadi sasa wachezaji wao wanne wanaoongoza kwa mabao ni Emmanuel Okwi, aliyefunga mabao 12 akiwazidi wachezaji wote VPL, Bocco anafuatia akiwa nayo tisa, huku Asante Kwasi na Shiza Kichuya kila mmoja akiwa nayo sita.

Tofauti ya alama 

Utamu na ukali wa mchezo huo unaongezwa kutokana na kuhusisha timu mbili zinazofuatana kwa ukaribu kwenye vita ya kuwania taji la ligi hiyo, Azam FC ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 33 huku Simba ikiwa kileleni ikijikusanyia 38.

Wakati Azam FC ikitoka kuichapa Ndanda mabao 3-1 kwenye mchezo uliopita wa raundi ya 16 ya ligi hiyo, Simba nayo imeipiga Ruvu Shooting 3-0, matokeo yanayofanya timu zote hizo mbili kuingia uwanjani zikiwa na morali kubwa.

Ushindi wowote wa Azam FC utaisaidia na kufanya kuzidi kuisogelea zaidi Simba kwenye mbio hizo na kubakisha pengo la pointi mbili, ushindi kwa wapinzani wao hao utazidi kuongeza muachano wa pointi na kufikia nane.

Mechi nyingine. 

Mbao FC v Singida United - CCM Kirumba, Mwanza.

Stand United v Lipuli FC - CCM Kambarage, Shinyanga.

Mwadui v Mtibwa Sugar - Mwadui Complex, Shinyanga.

Majimaji v Tanzania Prisons - Majimaji, Ruvuma.

Ndanda v Mbeya City - Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Related news
related/article
International News
Ronaldo: Cristiano and Neymar would be good together at Madrid
25 May, 14:45
International News
UEFA CL: Two arrested in Kiev after clashes before final
25 May, 14:16
International News
Ancelotti delighted with return
24 May, 08:55
International News
Pochettino signs new deal with Tottenham
25 May, 08:10
International News
FA condemns assault of match official
24 May, 20:18