VPL: Chirwa apiga tatu, Yanga wakimdhalilisha Njombe Mji

VPL: Chirwa apiga tatu, Yanga wakimdhalilisha Njombe Mji

06 Feb, 17:54

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara Dar Young Africans wamefanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji katika mchezo uliopigwa katika Dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam.

Yanga ambao wanakabiliwa na majeruhi ya wachezaji takribani 11 walipewa nafasi ndogo ya kuibuka na ushindi katika mchezo lakini mambo yalikuwa tofauti.

Katika dakika ya Tatu Raphael Daud alipiga V-Pass kuelekea langoni mwa Njombe Mji lakini walinzi walisimama imara na kuondoa hatari hiyo.

Dakika ya sita walinzi wa Njombe Mji walijichanganya na kuruhusu Obrey Chirwa kuweza kutumbukiza mpira wavuni lakini line one Khalfan Sika akanyanyua kibendera kuashiria ilikuwa ni offside.

Njombe Mji Walianza kucheza pasi fupifupi ili kuwachanganya wachezaji wote Yanga lakini Mara kadhaa walikuwa wakijisahau na kuacha Gadiel Michael kupiga pasi ambazo mara zote zilikuwa zikipotea bure.

Shuti la Emmanuel Martin 

Wakijiona kama tayari wameshawaweza Yanga, dakika ya 25 Emmanuel Martin alimjaribu kipa Rajabu Mbululu kwa shuti kali nje ya 18, shuti ambalo lilionekana kumshinda lakini walinzi wake wakafanikiwa kuondosha hatari.

Njombe Mji walijibu mapigo kwa shuti kali la guu la kulia la Ditram Nchimbi dakika chache baadae lakini kipa Ramadhan Kabwili akaudaka kirahisi.

Uimara wa Kabwili 

Njombe Mji walitulia na kupanga mashambulizi mengine, Heririmana Lewis akapokea pasi kutoka kwa Ditram Nchimbi na kuachia fataki lililopanguliwa na Kabwili na kuwa kona tasa.

Mpaka dakika 45 za mwamuzi Hans Mabena zinamalizika katika uwanja wa Uhuru, Yanga walikuwa mbele kwa umilikaji wa mpira (52%) wakati Njombe Mji wakiongoza kwa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango la Yanga mashuti manne kati ya nane.

Yanga hawakuchelewa walipoingia kipindi cha pili, kwani ilichukua dakika moja tu kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Obrey Chirwa ambaye alipokea pasi kisu kutoka kwa Pius Buswita.

Dakika ya 48 Njombe Mji walipata faulo nje kidogo ya 18, na kuchongwa na Etienne Ngiladjoe, ikionekana kama inaingia wavuni Ramadhan Kabwili akaupangua mpira na kuwa kona butu.

Kadi nyekundu. 

Njombe Mji walipata pigo katika dakika ya 54 baada ya mlinda mlango wao Rajabu Mbululo kupewa kadi nyekundu kwa kudaka mpira nje ya eneo lake baada ya kurudishiwa kwa kichwa na Ahmed Adewale.

Benchi la ufundi ikawabidi kumtoa Claide Wigenge na kuingia kipa David Kisu, huku Yanga nao wakatumia nafasi hiyo kwa kumtoa Raphael Daudi na kumuingiza Juma Mahadhi.

Yanga waliandika bao la pili kupitia kwa Obrey Chirwa katika dakika ya 65 kwa njia ya penati baada ya mlinzi Ahmed Adewale kunawa mpira ndani ya 18 akijaribu kuokoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni.

Bao la tatu

Kama hiyo haitoshi Yanga waliongeza bao la tatu katika dakika ya 69, juhudi kubwa za Juma Mahadhi ambaye alitokea kushoto mwa lango la Njombe na kupiga shuti ambalo liligonga besela na kumkuta Emmanuel Martin ambaye akamalizia kwa urahisi akimchambua kipa David Kisu.

Hat Trick 

Yanga waliandika bao la nne katika dakika ya 87 kupitia kwa Obrey Chirwa, akipokea Mpira ulioanzia kwa Pius Buswita na kumkuta Baruhani Akilimali ambaye bila uchoyo akampasia Chirwa na kufunga kirahisi.

Bao hilo la tatu kwa Chirwa katika mchezo huo yaani Hat trick, inamfanya kuwa mchezaji pekee ambaye amefanya hivyo mara mbili msimu huu.

Hat trick ya kwanza Chirwa kuipata ilikuwa katika mchezo dhidi ya Mbeya City ambao Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 mchezo ambao ulifanyika katika uwanja huo huo wa Uhuru.

Ushindi huo unakuwa ni wa tatu mfulululizo kwa Yanga na kufanya kufikisha alama 34 na kuchumpa hadi nafasi ya pili wakisubiri matokeo ya mchezo wa Jumatano kati ya Simba na Azam.

Yanga: Ramdhani Kabwili, Gadiel Michael, Hassan Kessy, Kelvin Yondani, Juma Makapu, Maka Edward, Pius Buswita, Papy kabamba, Obrey Chirwa/Said Mussa, Raphael Daud/ Juma Mahadhi na Emmanuel Martin/Baruan Akilimali.

Akiba: Beno Kakolanya, Said Musa, Yusuf Mhilu, Buruan Akilimali, Juma Mahadhi na Matheo Anthony.

Njombe Mji: Rajabu Mbululu, Agathon Mapunda, Harerimana Lewis, Ahmed Adewale, Raban Kambole, Aden Chepa, Willy Mgaya, Juma Mpakala, Etienne Ngiladjoe, Ditram Nchimbi na Claide Wigenge/David Kissu.

Akiba: David Kissu, John Sagala, Mack Mwambungulu, Jimmy Mwasongola, Raphael Siame, David Obash na Nickson Kibabage.

Mechi za Februari 7.

Simba SC v Azam - Taifa, Dar.

Mbao FC v Singida United - CCM Kirumba, Mwanza.

Stand United v Lipuli FC - CCM Kambarage, Shinyanga.

Mwadui v Mtibwa Sugar - Mwadui Complex, Shinyanga.

Majimaji v Tanzania Prisons - Majimaji, Ruvuma.

Ndanda v Mbeya City - Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Related news
related/article
International News
CL Final:Liverpool boss expects his side to be brave
6 hours ago
International News
New Arsenal boss Unai Emery's top five past signings
25 May, 09:00
International News
Former Spain coach showers praise on Real Madrid
23 May, 09:00
International News
New Arsenal boss Unai Emery's top five past signings
25 May, 09:00
International News
Fairytale ending could be in the script, says World Cup-bound Vardy
24 May, 14:24