CECAFA 2017: Zanzibar waikamata koo Kilimanjaro Stars

CECAFA 2017: Zanzibar waikamata koo Kilimanjaro Stars

07 Dec 2017, 15:55

Timu ya Taifa ya Soka ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' imeendeleza ubabe katika michuano inayosimamiwa na Baraza la vyama vya soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati 'CECAFA' Kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya ndugu zao Tanzania Bara.

Zanzibar wakicheza kandanda la kuvutia katika uwanja wa Kenyatta uliopo Kaunti ya Machakos nchini Kenya, walitoka nyuma kwa bao moja na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo ambao umewapeleka kileleni mwa Kundi A.

Katika dakika 20 za mwanzo Zanzibar Heroes walikuwa bora zaidi ya Kilimanjaro Stars wakishambulia Kwa makini na kutengeneza nafasi nyingi zaidi.

Aidha kuumia kwa Kelvin Patrick Yondani na kuingia kwa Boniface Maganga kulisababisha eneo la kati la Kilimanjaro Stars kupwaya na kuruhusu mashambulizi mengi kupitia kwa Mohamed Issa na Hamad Mshamata.

Kama hiyo haitoshi dakika ya 7 kiungo wa Zanzibar Heroes anayeichezea Mtibwa Sugar Mohamed Issa alipiga shuti kali ambalo kama si umakini wa Aishi Manula, Zanzibar wangeandika bao la kuongoza.

Dakika 9 baadae Hamad Mshamata alipata nafasi ya wazi ya kuandika bao kwa Zanzibar Heroes lakini shuti lake lilidakwa na Kipa Aishi Manula na kufanya mambo kuwa suluhu hadi muda huo.

Bao la Himid Mao. 

Himid Mao Mkami akaiandikia Kilimanjaro Stars bao la kuongoza katika dakika ya 28 baada ya kupokea pasi kutoka Danny Lyanga kushoto mwa lango la Zanzibar Heroes.

Bao hilo lilifanya benchi la ufundi la Zanzibar Heroes kufanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumtoa mshambualiaji Hamad Mshamata na kumuingiza kiungo Seleman Kasimu Selembe.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Kilimanjaro Stars kuwa mbele kwa bao 1-0 bao ambalo lilifungwa na Himid Mao Mkami, na pindi timu ziliporejea kwa ajili ya kipindi cha pili Kili Stars walibadilika na kuanza kulishambulia lango la Zanzibar Heroes kama nyuki.

Mashambulizi hayo hayakudumu sana baada ya Zanzibar Heroes kuusoma mchezo na kuwabana Kili Stars na kuufanya mchezo kuwa 50/50 kwa timu zote mbili.

Mudathir Yahya akiwa yeye na kipa katika dakika ya 56 anapiga Nje na kushindwa kuisawazishia Zanzibar Heroes, kosakosa hiyo inamfanya kocha Hemed Suleiman kufanya mabadiliko kwa kumtoa Mudathir na kumuingiza Kassim Suleiman Khamis.

Bao la Kassim Suleiman. 

Mabadiliko hayo yalisaidia ambapo katika dakika ya 66, akiambaa na mpira upande wa Kulia mwa lango la Kili Stars, Kassim Suleiman Aliweza kumpiga chenga Boniface Maganga na kumuangalia kipa Aishi Manula alivyokaa na kupiga shuti lililozaa bao la kusawazisha.

Bao hilo liliwashtua Kilimanjaro Stars na kusababisha benchi la ufundi kufanya mabadiliko kwa kumtoa Abdallah Hamisi na kumuingiza Jonas Mkude, aidha Elius Maguri alitoka na kuingia kinda Yahya Zayd. 

Bao la Ibrahim. 

Mabadiliko hayakusaidia chochote na hayakuweza kuwazuia Zanzibar kuandika bao la pili, ambapo mpira uliochongwa Magharibi  mwa lango la Stars ulimkuta Kassim Selembe ambaye naye akampasia Ibrahim Hamad Ilika na kuandika bao la pili. 

Hadi kipyenga cha mwisho kinapulizwa Zanzibar Heroes walitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya ndugu zao Tanzania Bara ambao walipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo. 

Zanzibar vinara. 

Matokeo hayo yanawafanya Zanzibar Heroes kufikisha alama 6 katika michezo miwili waliyocheza na kuongoza kundi A, wakati Tanzania Bara wakisaliwa na alama moja baada ya michezo miwili.

Katika ratiba ya michuano hiyo Tanzania Bara wanakuwa wamebakiwa na michezo miwili dhidi ya Rwanda na ule wa kumaliza michezo ya Kundi dhidi Kenya, wakati Zanzibar wao wakitarajiwa kucheza na Kenya na baadae kumaliza na Libya.

Related news
related/article
FIFA World Cup
Modric backed for Golden Ball award
10 Jul 2018, 11:15
English Premier League
Lazaridis calls for striking improvements at West Ham
10 Jul 2018, 10:35
English Premier League
Silva hopes Everton will deliver on transfer targets
1 hour ago
FIFA World Cup
Drama as pitch invaders interrupt World Cup final
16 hours ago
Ligue 1
Buffon beaten on PSG debut
20 hours ago