Watanzania na majukumu yao nje ya nchi, matokeo na ratiba.

Watanzania na majukumu yao nje ya nchi, matokeo na ratiba.

15 Oct, 08:46

Ni wikiend nyingine kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye soka la Kimataifa wakitafuta njia na tiba za kuzisaidia timu zao kuweza kufanya vizuri na hatimaye kufikia malengo yao.

Jumamosi ya Oktoba 14 Mtanzania Mbwana Samatta alikuwa dimbani kuisaidia Timu yake ya KRC Genk kuchukua alama tatu dhidi ya Royal Excel Mouscron lakini mambo yakawa magumu na kujikuta wakitoka sare ya bao 1-1.

Mchezo huo ambao ulipigwa katika uwanja wa Nyumbani wa Genk, Luminus Arena ulishuhudia Samatta akipiga dakika zote 90, lakini alishindwa kabisa kuisadia timu yake ambayo ndio ilikuwa ya kwanza kufungwa katika dakika ya 42 kupitia kwa Dorin Rotariu kabla ya kusawazisha katika dakika ya 81 kupitia kwa Marcus Ingvartsen.

Sare hiyo inawafanya Genk ambao tayari wamecheza michezo 10, kuwa Nyuma ya alama 13 dhidi ya kinara wa ligi hiyo kwa sasa Club Brugge ambaye anaongoza akiwa na alama 24.

Unaweza kuwa msimu mbaya sana kwa Mbwana Samatta kwani toka kuanza kwa Ligi wameshinda michezo miwili pekee, wakitoka sare mara tano na kufungwa mara 3, dalili ambayo inawaondoa kabisa kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Aidha msimu uliopita Mbwana Samatta alimaliza ligi akiwa na mabao 13 lakini msimu huu amefanikiwa kufunga mabao matatu mpaka sasa.

Michael John Lema.

Watanzania wengine watazitumikia timu zao leo Jumapili ambapo katika ligi kuu ya Austria maarufu kama Bundesliga Timu ya Michael John Lema, Strum Graz itakuwa na kibarua kigumu majira ya saa 11:30 jioni pale itakapowakaribisha wakongwe Austria Wien.

Graz watahitaji ushindi katika mchezo ili kuwatoa Salzburg kileleni, ambao walishinda jana dhidi LASK na kufikisha alama 24, alama mbili zaidi ya zile walizonazo Strum Graz.

Kenya.

Nchini Kenya Watanzania Abdlah Hamis na Abdul Hilal watakuwa vibaruani kupeperusha bendera ya Tanzania katika harakati za kutafuta alama tatu muhimu katika Timu zao.

Abdlah Hamisi anayeichezea Sony Sugar watakuwa na mchezo mkali dhidi ya Nzoia Sugar FC ikiwa ni Dadi ya sukari. 

Sony Sugar wanashuka dimbani katika mchezo huo wakiwa na alama 34 na kukalia katika nafasi ya 10 ilihali wapinzani wao Nzoia Sugar wao wakiwa nafasi ya 8 huku wakiweka kibindoni alama 39.

Mtanzania Mwingine Abdul Hilal anayeichezea Tusker FC atakuwa na kibarua kigumu pale timu yake itakapokuwa na shughuli pevu ya kuwakabili vijana wa Muhoroni Youth.

Tusker ambao ni mabingwa watetezi hawapo katika nafasi nzuri huku ligi hiyo ikiwa katika duru la lala salama, ambapo mpaka sasa wakiwa wamecheza michezo 27 wamekusanya alama 40 pekee, huku wakiwa katika nafasi ya 7.

Morocco.

Kule Moroko kwake Simon Msuva, watakuwa na mchezo wa Ligi leo ambapo Difaa El Jadida watakuwa nyumbani kuwakaribisha Chabab Rif Hoceima.

El Jadida wanaenda katika mchezo wakiwa wana alama 4 katika michezo miwili ambayo wamecheza hadi hivi sasa katika ligi hiyo ya Moroko.

Afrika Kusini.

Kwake Abdi Banda pamoja Kipa Deogratius Munish wenyewe watakuwa na Mapumziko mafupi wikiendi hii, wakitarajiwa kuanza tena mikimiki ya ligi kuu ya Afrika Kusini Oktoba 17.

Banda anayeichezea Baroka FC wenyewe watakuwa na mchezo siku ya Oktoba 18, na watacheza na Lamontville Golden Arrows.

Ikumbukwe Baroka ndio wanaongoza Ligi wakiwa na alama 15 baada ya michezo 7 wakishinda 4 na wakitoka sare katika michezo 3.

Wakati Deogratius Munish yeye atakuwa mzigoni kuisaidia timu yake ya Tuks FC inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Pretoria, timu hiyo inashiriki ligi daraja la Kwanza.

Msumbiji.

Naye Uhuru Suleiman anayeichezea União Desportiva do Songo ya Msumbiji Leo watakuwa na mchezo wa kumalizia malizia ligi hiyo maarufu kama Mocambola dhidi ya Chibuto. 

Tayari timu ya Songo anayoichezea Uhuru Suleiman imekwisha nyakua taji la ligi hiyo msimu huu Kwani mpaka sasa ina Alama 62 huku timu zikiwa zimesaliwa na michezo miwili kukamilisha ligi hiyo. 

Mchezo huo utapigwa majira ya saa 10 jioni kwa saa za Msumbiji huku Tanzania ikitarajiwa kuwa ni saa 11 jioni. 

Related news
related/article
International News
Fred to keep United waiting
25 May, 08:55
International News
Andres Iniesta's nine LaLiga triumphs with Barcelona
24 May, 13:05
International News
UEFA CL: Road to Kiev
23 May, 19:00
International News
Ronaldo: I can't be compared with Salah
25 May, 14:25
International News
Madrid ace not interested in PL move
25 May, 14:05