Ratiba ya ligi kuu raundi ya 17, Simba kucheza na kibonde wa Yanga

Ratiba ya ligi kuu raundi ya 17, Simba kucheza na kibonde wa Yanga

05 Feb, 09:08

Mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania Bara raundi ya 17 inatarajiwa kuendelea Jumanne ya Februari 6 kwa mchezo mmoja ambapo mabingwa watetezi Dar Young Africans watakuwa nyumbani katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kucheza na Njombe Mji.

Yanga ambao wanashika nafasi ya tatu wakiwa na alama 31 wataendelea kuwakosa wachezaji wao muhimu takribani 11 watakaposhuka dimbani katika mchezo huo.

Katika mchezo uliopita baina ya timu hizo mbili uliofanyika katika uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 bao ambalo lilifungwa na Ibrahim Ajib kwa faulo ya moja kwa moja.

Aidha Njombe Mji wao wanashuka katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita kwa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons na kuzidi kudidimia mkiani mwa msimamo wa ligi wakiwa na alama 13 katika nafasi ya 16.

Simba v Azam 

Ligi hiyo itaendelea Jumatano ya Februari 7 ambapo siku hiyo kutakuwa na michezo saba itakayorindima katika viwanja mbalimbali nchini.

Mchezo mkali na unaosubiriwa kwa hamu kubwa ni ule utakaowakutanisha mabingwa mara 18 Simba SC na mabingwa mara moja Azam FC.

Mwaka huu timu hizo zilikutana katika mashindano ya mapinduzi yaliyofanyika visiwani Zanzibar na Azam kuibuka na ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Idd Kipagwile.

Aidha wanakutana kwenye ligi huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka Sare ya 0-0 katika mchezo wa Mzunguko wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar.

Kila timu inahitaji ushindi, mathalani Azam watahitaji pointi tatu ili kupunguza wigo wa alama kutoka tano hadi mbili wakati Simba kama watashinda wataongeza wigo wa alama nane na Azam waliopo katika nafasi ya pili.

Mbao v Singida Utd 

Mechi nyingine kali siku hiyo ya Jumatano itawakutanisha Singida United waliopo katika nafasi ya 4 na alama zao 30 dhidi ya Mbao FC Waliopo katika nafasi ya 7 na alama zao 18.

Mchezo huo mkali utafanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati ambapo Mbao wametoka kuifunga Kagera Sugar kwa mabao 2-1.

Stand v Lipuli 

Wanapaluhengo Lipuli FC wao wamesafiri hadi mkoani Shinyanga kucheza na Chama la wana Stand United katika uwanja wa CCM Kambarage.

Lipuli haina matokeo mazuri kwa siku za hivi karibuni wakifungwa michezo mitatu mfulululizo katika uwanja wao wa nyumbani huku Stand United wao wakiwa moto licha ya kupoteza mchezo mmoja katika michezo mitatu iliyopita ya ligi.

Mwadui v Mtibwa 

Mtibwa Sugar baada ya kufungwa na Stand United watakuwa na nafasi ya kujiuliza mbele ya wachimba Almas Mwadui FC ambao wao wanakumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Singida United.

Mchezo huo mkali na muhimu kwa pande zote mbili utafanyika kwenye uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.

Majimaji v Prisons 

Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya watasafiri hadi mkoani Ruvuma ambapo huko watakutana na Wanalizombe Majimaji FC.

Majimaji katika mchezo uliopita wamepoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City hivyo watahitaji ushindi ili kuongeza matumaini ya kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja wakati huohuo Tanzania Prisons wao wametoka kuifunga Njombe Mji na pengine wakawa na morali zaidi ya kupata matokeo mazuri.

Ndanda v Mbeya City 

Wanakuchele Ndanda FC watawakaribisha Wanakomakumwanya Mbeya City timu inayomilikiwa na halmashauri ya jiji la Mbeya katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Ndanda wana alama 16 wakiwa katika nafasi ya 10 wakati Mbeya City wao wapo katika nafasi ya 8 wakiwa na alama 17 hivyo ni mchezo muhimu kwa timu zote katika harakati za kuimarisha nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.

Shooting v Kagera 

Mechi ya mwisho siku hiyo itakuwa kati ya Ruvu Shooting watakaopambana na Kagera Sugar ambao msimu huu wapo dhohofu ili hali.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika katika Dimba la Mabatini lililopo Mlandizi mkoani Pwani na ikumbukwe katika mchezo uliopita baina yao timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Simba bado wanaendelea kuongoza wakiwa na alama 38 wakifuatiwa na Azam wenye alama 33 nao Yanga ni watatu wakiwa na alama 31 wakati Singida United ni wanne wakiwa na alama 30.

Mkiani wapo Majimaji, Kagera Sugar na Njombe Mji ambao wote wana alama 13 na ikumbukwe msimu zitashuka timu mbili badala ya tatu ili kupisha timu sita kutoka ligi daraja la kwanza.

Related news
related/article
International News
Football legend set to marry two women at same time
24 May, 12:40
International News
Suarez: Iniesta hard to replace at Barcelona
24 May, 08:15
International News
Rwanda to sponsor Arsenal's new sleeve
23 May, 09:05
International News
Scholes: Manchester United should sell Pogba
24 May, 10:45
International News
Andres Iniesta's nine LaLiga triumphs with Barcelona
24 May, 11:05